Habari

MKURUGENZI TCRA ATHIBITISHA UWEPO WA TATIZO LA KIMTANDAO NCHINI

    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari amesema tatizo la Mtandao kukwama siku ya leo imetokana na Miundombinu ya Intaneti na sio kifaa unachokutumia (Simu).

     " Kunaonekana kuna tatizo la kiufundi kidogo linalohusiana na 'marine cables' kwa hiyo tunajaribu kupata maelezo zaidi," amesema Dk Bakari.

    Dk Bakari amesema kwa sasa wanatazama namna ya kupata taarifa zaidi ili kujua ilipo changamoto ili kuchukua hatua.

MANISPAA YA LINDI YAINGIA MAKUBALIANO YA BIASHARA YA HEWA UKAA

      Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Lindi  limepitisha mkataba wa makubaliano ya Biashara ya hewa ukaa katika vijiji 10 , jumuhiya za uhifadhi wa Misitu 3  na msitu wa hifadhi wa manispaa na kampuni ya village climate solution limited (VCSL).

       Wakizungumza katika kikao cha robo ya tatu ya baraza hilo ,  madiwani  hao wamesema kuwepo kwa biashara hiyo kutaiongezea Halmashauri chanzo kipya cha mapato na kwamba mradi huo utakuwa na manufaa kwa Manispaa na wananchi kwa ujumla

DKT.MWINYI AKUTANA NA ASKOFU MKUU WA ANGLIKANA DUNIANI

     Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa la Kianglikana na Taasisi nyingine za dini kwa kudumisha amani na utulivu .

      Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipokutana na Kiongozi wa Kanisa la Kianglikana Duniani , Askofu  Mkuu Justin Welby na ujumbe wake waliofika Ikulu Zanzibar tarehe 11 Mei 2024.

     Rais Dk.Mwinyi amemshukuru Askofu Justin Welby kwa ujio wake  Zanzibar.

DKT.MWINYI AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUJA KUWEKEZA NCHINI

      Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema  Zanzibar ina miradi mingi inayohitaji Wawekezaji kuja kuwekeza.

     Katika mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara na Reli  CCECC kutoka China amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kushirikiana na Kampuni hiyo kutimiza ndoto ya kuijenga upya Zanzibar. 

MAMA MARIAM MWINYI ATOA SHUKURANI KWA SERIKALI YA KOREA

     Mke wa Rais wa Zanzibar , Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF)  Mhe.Mama Mariam Mwinyi ameishukuru  wadau wa maendeleo wa Korea kupitia Jumuiya ya Lady Fatima Charity kwa msaada  wa dola za kimarekani 37,000  kwa ajili kuwezesha upatikanaji wa  kutoa Taula za kike (Tumaini Kits)  zinazotengenezwa na ZMBF na zimenufaisha zaidi ya Wasichana 2500 wa shule za Pemba.

WAZIRI TABIA AWAOMBA VIONGOZI PAMOJA NA WANANCHI KUSHIRIKIANA KATIKA MAPOKEZI YA MBIO ZA MWENGE

     Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewaomba viongozi, wafanyakazi, vikosi vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kushiriki katika mapokezi ya mbio za mwenge mwaka 2024.

      Mhe. Tabia ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na mapokezi ya mbio za mwenge wa uhuru kwa upande wa Zanzibar.

     Amesema mwenge wa uhuru mwaka 2024 kuwasili Zanzibar tarehe 13 mei 2024 na kutembezwa katika Mikoa na Wilaya zote za Unguja na Pemba.

PAC YATOA PONGEZI KWA WIZARA YA UJENZI

     Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuandaa andiko la mkakati wa kuwawezesha makandarasi wazawa na washauri elekezi kwenye utekelezaji wa miradi ya Ujenzi na kusisitiza andiko hilo kushirikisha wataalamu kutoka Sekta mbalimbali nchini ili kuweza kuleta tija kwa Taifa.

ZFCT YATAKIWA KUSHUKA KWA WANANCHI ILI WAWEZE KUFAHAMIKA IPASAVYO

     Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban ameliagiza Baraza la ushindani halali wa Biashara Zanzibar (ZFCT) kushuka chini kwa wananchi ili waweze kulifahamu na kuweza kulitumia kama linavyotakiwa.

     Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Zura Maisara wakati alipokuwa akizinduwa Baraza la pili la Ushindani halali wa biashara Zanzibar.

ELIMU YA HAKIMILIKI KUTOLEWA KWA VIJANA MILLIONI MOJA

     Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU) na taasisi ya Ruge Mutahaba Foundation kufanya Kampeni ya kutoa Elimu ya Hakimiliki.

    Akizungumza kuhusu Kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa COSOTA Bi. Doreen Sinare amesema itatambulika kama "HAKIMILIKI YAKO HAILIKI, KAMATA FURSA TWENZETU"

     Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi Mei 09, 2024 Jijini Dar es Salaam katika siku ya Maadhimisho ya Miliki Ubunifu Duniani.

SMT NA SMZ KUIMARISHA TAASISI ZA UJENZI ZA NDANI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuweka Mazingira mazuri kwa kuziimarisha Taasisi za Ujenzi ili kuhakikisha Wataalamu wazawa wanakuza Taaluma zao na kushiriki katika Ujenzi wa Miradi inayojengwa na Watanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla yamesemwa hayo alipofungua mafunzo ya kuwaendeleza Wataalamu wa Usanifu, uhandisi na Wakadiriaji Majengo Tanzania huko Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Subscribe to Habari
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.