Habari

WAZAZI NA WALEZI MKOANI LINDI WATAKIWA KUTUMIA MIFUMO RASMI KATIKA KUMALIZA MIGOGORO YAO

   Wazazi na walezi Mkoani Lindi wametakiwa kuitumia vyema mifumo iliyowekwa na Serikali katika kushughulikia migogoro na tofauti zinazojitokeza katika familia zao  ambayo kwa kiasi kikubwa uchangia kuachana na  kusababisha watoto kuathiriwa kwa kukosa  malezi imara.

    Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo  katika maadhimisho ya siku ya Familia ambayo kwa ngazi ya Mkoa yamefanyika katika viwanja vya soko la majengo halmashauri ya Mtama Mkoani humo.

WALIMU WATAKIWA KUFUATA MAADILI YA KAZI YAO

     Mkaguzi kata ya Lwenzera Wilaya ya Geita Mkoani Geita amewataka Walimu Wa Shule ya Sekondari Bugando Kufuata Maadili ya Kazi huku akiwataka kutambua kuwa Jamii inawategemea katika kuwafundisha na kutoa malezi Mema kwa Wanafunzi.

     Hayo yamebainishwa na Mkaguzi wa Kata hiyo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi A/INSP, Pili Kulele wakati alipotembelea Shule hiyo ambapo amewaomba walimu kujikita katika kuwafundisha wanafunzi na kutoa malezi mema ili wawe msaada katika Jamii na kata hiyo kwa ujumla.

WAZIRI WA BIASHARA AAHIDI KUTOA MASHIRIKIANO KWA BARAZA LA UDHIBITI MFUMO WA UTOAJI LESENI

    Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe.Omar Said Shaaban ameahidi kutoa ushirikiano kwa Baraza la Udhibiti Mfumo wa Utowaji wa Leseni ili kufikia malengo ya kuweka mazingira mazuri ya kibiashara nchini.

    Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Baraza la Udhibiti Mfumo wa Utowaji wa Leseni katika ukumbi wa Ofisi za Baraza huku Malindi, Wilaya ya Mjini.

SIKU SABA SERIKALI KUTOA MAAMUZI UWEPO WA SOKO LA MAADINI YA VITO TUNDURU

     Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema ndani ya siku saba kuanzia Mei 15,2024,serikali itatoa maamuzi ya uwepo wa soko moja au masoko matatu ya madini ya vito wilayani Tunduru.

    Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea,Kanali Abbas amesema akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Tunduru hivi karibuni aliweza kutembelea masoko ya madini ya  vito ambayo ni soko la Generation,TUDECU na kukagua ujenzi wa soko jipya la madini.

SERIKALI IMEPIGA HATUA SEKTA YA ANGA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Wadau wa Sekta ya Anga kuimarisha Mashirikiano ili kuhakikisha Sekta hiyo inazidi kuimarika.

Akifungua Kongamano la Sita la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki  katika Hoteli ya Verde Mtoni,Dk.mwinyi, amesema Nchi inajivunia mafanikio yaliofikiwa katika sekta hiyo.

VIONGOZI NA WAKUU WA TAASISI WAMESISITIZWA KUSIMAMIA UWAJIBIKAJI.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais katiba Sheria, Utumishi na Utawala bora Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema ni jukumu la wakuu wa Taasisi na vitengo kukaa pamoja kujadili namna ya kuwaelimisha Watendaji wao juu ya utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma.

VIJANA NA WANAFUNZI WAMETAKIWA KUTUMIA VYEMA MITANDAO YA KIJAMII

Naibu Waziri wa maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Anna Athanas Paul  amewasisitiza  Vijana na Wanafunzi Kutojirikodi na kujirusha katika Mitandao ya Kijamii  ili kujiepusha na Matatizo yatakayo jitokeza.

Akizungumza katika Madhimisho ya Siku ya Familia Duniani Naibu Waziri huyo amesema ili kulinda Maadili na Malezi bora kwa Watoto ni vyema kwa Wazazi kuwasimamia Watoto pamoja na kuwasisitiza Vijana  kuacha Tabia za  kujituma katika Mitandao ya Kijamii na badala yake kuitumia kwa kuwaletea Faida.

ASKARI JKU WAMEHIMIZWA UWAJIBIKAJI NA UFANISI

Mkuu wa Jeshi la kujenga Uchumi (JKU), Kanal Makame Abdallah Daima, amewataka Wafanyakazi wa Jeshi hilo kufanyakazi kwa bidii na Ufanisi, kwa lengo la kuisaidia Serikali katika kuimarisha Uchumi.

Mkuu huyo wa JKU ameyasema  hayo Chuo cha Uongozi JKU Dunga wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Jeshi hilo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo ikiwa ni muendelezo wa kukumbushana kuhimizana  Majukumu yao ya Kazi ya kila siku ndani ya Jeshi hilo.

WANANCHI WAMETAKIWA KUPIMA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

Wanawake wenye umri kuanzia Miaka 18 hadi 69 wametakiwa kujitokeza kwenye upimaji wa Saratani ya shingo ya Kizazi katika Hospitali ya Mnazi Unguja Mmoja na Chakechake Kisiwani Pemba

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt Amour Mohamed Suleiman alipokuwa akizungumza na Timu ya Madaktari kutoka China wanaotarajiwa kuanza zoezi la upimaji wa Saratani ya shingo ya Kizazi hapa Zanzibar.

NCHI ZA KANDA YA AFRIKA MASHARIKI KUSHIRIKIANA KATIKA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA HALI YA HEWA

    Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari ametoa rai kwa wataalamu kutoka nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuboresha ushirikiano ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza hususani kipindi cha matukio ya hali mbaya ya hewa.

     Mhe. Mshibe alisema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Kamati ya Usimamizi wa Programu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa kwa nchi Wanachama Kanda ya Afrika Mashariki, unaofanyika Dar es Salaam, 14-17 Mei, 2024.

Subscribe to Habari
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.