Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ina mpango wa kujenga Nyumba za Madakatari kila Wilaya ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.
Dkt. Mwinyi ameeleza hayo huko Hospitali ya Abdulla Mzee Wilaya ya Mkoani wakati wa uwekaji wa Jiwe la msingi kwenye Nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali hio ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za kutimiza miaka sitini (60) ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema Serikali imeona upo umuhimu wa kuwajengea na kuwaimarishia Makazi Madaktari hao kwa kuwajengea Nyumba zenye hadhi bora ambazo zitarahisisha na kuongeza ufanisi wa Utendaji wao.
Amewahakikishia Wananchi kuwa Serikali ina mpango wa kujenga Hospitali za Rufaaa kwa kila Mkoa wa Zanzibar zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya Wananchi katika suala la upatikanaji wa huduma bora za afya.
Akizungumzia suala la mfumuko wa bei hasa kuongezeka kwa bei za bidhaa, Dkt. Mwinyi, amesema Serikali imeshaliagiza Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kuagiza Chakula nje ya Nchi ili kuleta nafuu ya bei na kuongeza upatikanaji wa chakula cha kutosha kitakachokidhi mahitaji ya Wananchi.
Naibu Waziri wa afya wa Zanzibar Mhe Hassan Hafidh ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuwajengea Wananchi Hospital za kisasa kwa kila Wilaya ambazo husaidia kupunguza usumbufu kwa Wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.