Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa kuzingatia misingi ya haki na uadilifu na kulipa kodi ili Serikali iweze kukusanya Mapato na kuendelea kutoa huduma bora kwa Jamii.
Dkt. Mwinyi amesema hayo alipofungua Mkutano Mkuu wa kumi na tano (15) wa Kitaifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar, huko Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar amesema kufanyika biashara kwa misingi hiyo itaweza kutoa huduma mbali mbali za maendeleo kwa Wananchi ikiwemo afya bora, Barabara na huduma za elimu.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya ya Wafanyabiashara kwani Jumuiya hiyo ni muhimili muhimu katika kuimarisha na kufanikisha maendeleo ya Biashara Zanzibar.
Aidha dkt Mwinyi ameitaka jumuiya hiyo kuitangaza Zanzibar Kimataifa huku akisisitiza kuyafanyia kazi makubaliano ya Mikataba wanayoingia na mashirika ya Kimataifa kwa kutafuta ufanisi ili kuleta maendeleo ya haraka Nchini.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Biashara Zanzibar Mhe. Omar Said Shaban amaesema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kutunga Sheria ya kuifanya Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar kuwa ni Mwemvuli wa Jumuiya zote za Wafanyabiashra wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Zanzibar Ali Amour amesema jumuiya hiyo inakusudia kuyafanyia kazi matatizo yanayoikabili Jumuiya na Wafanyabiashara ili kuwa ni sehemu ya mafanikio kwa Wafanyabiashara wa Zanzibar.
Afisa Mtendaji kutoka Tanzania Commercial Bank ambaye ni Mdhamini Mkuu wa mkutano huo Adam Mihaya ameahidi kuendelea kushiriki kutoa huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo Sekta ya Utalii pamoja na kuwashukuru Watanzania kwa kuiamini Benki hiyo.