Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema uchumi wa Nchi yoyote Duniani hauwezi kujengwa na Sekta ya umma pekee bali ni lazima kushirikiana na Sekta Binafsi katika uwekezaji wa Miradi mbali mbali ya Kiuchumi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Bandari ya FUMBA ikiwa ni Shamra shamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi amesema Sekta Binabsi zina mchango mkubwa wa kuinua uchumi wa Nchi ambapo miongoni mwa vyanzo vya mapato ya Nchi ni Bandari hivyo ni vyema kwa serikali kuweka mikakati imara kuhakikisha inainua pato hilo na kuona Wananchi wake wanafaidika kupitia Bandari.
Dkt Mwinyi amefahamisha kuwa kwa sasa Bandari ya Malindi imekosa ufanisi kutokana na kuzidiwa kwa shughuli mbali mbali ikiwemo ongezeko la watu pamoja na kukuwa kwa biashara hivyo Serikali imeona ipo haja ya kujenga Bandari ya Fumba ili kutatua tatizo la kuchelewa kufika kwa Makontena hali inayosababisha kupanda kwa bei za Bidhaa.
Aidha amesema mategemeo ya Serikali ni kuimarisha Bandari za Abiria ikiwemo ya Mpiga duri pamoja na kutoa huduma za ziada kwa Wananchi.
Akitoa tarifa ya kitaalam Kepten Talib Khamis amesema zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 15 zimetumika katika ujenzi huo wa Bandari ya Fumba ambapo Bandari hiyo ina uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani zaidi ya 50.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dkt Khalid Salum Mohamed amesema kwa hivi sasa Zanzibar inashuhudiwa kuwa na maendeleo ya kila Sekta hivyo wananchi wanapaswa kupongeza huku akitoa shukrani kwa Dkt Mwinyi kwa hatua hiyo aliyoifanikisha katika Ujenzi wa bandari hiyo.