Zanzibar, 11 Februari 2026 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Ndugu Seif Abdalla Juma, ametoa ufafanuzi kwa umma kufuatia taarifa zilizosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari zikidai kuwa mamlaka hiyo imeshindwa kudhibiti matukio ya wizi wa mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA).

ZAA imekanusha rasmi taarifa hizo ikizieleza kuwa si sahihi na zinalenga kupotosha umma. Mamlaka imesisitiza kuwa haijawahi kutoa tamko lolote linalokiri kuwepo kwa vitendo vya wizi wa mizigo ndani ya uwanja huo. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, mamlaka ilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara waliodai kupotea au kufunguliwa kwa mizigo yao.
Kufuatia malalamiko hayo, na kutokana na eneo lililotajwa kuwa ni la ndani ya ndege (cargo hold) ambalo kwa kawaida halina kamera, ZAA iliunda kamati maalum iliyofanya uchunguzi wa kina kwa muda wa mwezi mmoja. Kamati hiyo ilikagua mizigo inayosafirishwa ndani ya ndege pamoja na mchakato wa upakuzi ili kubaini iwapo kulikuwa na dalili za ufunguaji wa mabegi au wizi. Aidha, zoezi maalum la ukaguzi lilifanyika kwa wahudumu wote wanaoingia ndani ya ndege kwa lengo la kuimarisha usalama.

Matokeo ya uchunguzi, yakisaidiwa na mapitio ya ushahidi wa picha na kamera za uchunguzi, yalibaini kuwa mizigo mingi iliyodaiwa kufunguliwa au kuharibika ilikuwa tayari katika hali hiyo kabla ya kuwasili Zanzibar. Hivyo, ZAA imesisitiza kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa vitendo vya wizi vinafanyika ndani ya eneo la uwanja wa ndege wa AAKIA.
Pamoja na hayo, mamlaka imechukua hatua za ziada za kiusalama ikiwa ni pamoja na kuwataka watoa huduma wa mashirika ya ndege (ground handlers) kufunga kamera maalum ndani ya ndege, pamoja na kuwapatia wapakuzi mizigo kamera za kuvaa mwilini (body cameras) ili kurahisisha ufuatiliaji wa mchakato mzima wa upakuzi na kubaini haraka mizigo inayoharibika.

ZAA imeeleza kuwa mifumo ya usalama inaendelea kuimarishwa mara kwa mara ili kuhakikisha viwango vya juu vya ulinzi kwa abiria, mizigo na mali za wadau wa usafiri wa anga vinazingatiwa wakati wote. Mamlaka pia imewaomba wananchi na wasafiri kuzingatia taratibu za usalama kwa kuepuka kuweka vitu visivyoruhusiwa katika mizigo ya kuingia nayo ndani ya ndege (check-in luggage). Aidha, imekumbusha kuwa mizigo inaweza kufunguliwa na Maafisa Usalama katika uwanja wa kuondokea endapo kutakuwa na viashiria vya hatari, kwa lengo la kujiridhisha na kuondoa tishio lolote kwa usalama wa ndege na abiria.

ZAA imewahimiza wananchi, wadau na vyombo vya habari kupata taarifa kupitia vyanzo rasmi ili kuepuka kusambaza habari ambazo hazijathibitishwa na zinazoweza kuathiri taswira ya uwanja pamoja na sekta ya usafiri wa anga kwa ujumla. Mamlaka imeongeza kuwa itaendelea kuwa wazi kupokea taarifa na malalamiko yote yanayohusu huduma zake ili yashughulikiwe kwa haraka, uwazi na ufanisi, huku ikihakikishia umma kuwa usalama wa mizigo na utoaji wa huduma bora katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume unabaki kuwa kipaumbele cha juu.

