Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amesema Mashindano ya Kuhifadhisha Qur-an yana mchango mkubwa katika kuwajenga Vijana Kimaadili, fikra na nidhamu pamoja na kumjua Mwenyezi Mungu.
Ameyasema hayo katika Uzinduzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur-an Tukufu uliofanyika katika Ukumbi wa Madinatul Bahar Mbweni Jijini Zanzibar.
Amesema kuwepo kwa Mashindano ya Qur-an yanawasaidia Vijana kujitenga na matendo maovu na macahfu kwa vile hutumia muda mwingi wa Kusoma na kujiandaa kushiriki katika Mashindano mbali mbali Ndani ya Nchi na Nje ya Nchi.
Alhajj Hemed amesema endapo Vijana hawatowekewa misingi imara ya kitabia na kuifahamu Dini yao watakuwa sirahisi kufuata tamaduni za kigeni ambazo zinakwenda kinyume na mila, silka na desturi za kizanzibari na kuikumbusha Jamii kuhimiza na kusimamia maadili mema kuanzia ngazi ya Familia, Skuli, Madrasa na maeneo ya ibada kuwasaidia Vijana na vizazi vijavyo kuishi katika mazingira ya Kumcha Mungu.
Amesema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na ZBC na Ofisi ya Mufti katika kujenga Jamii yenye Maadili mema, hivyo Serikali itaendelea kuunga Mkono harakati za Kidini ambazo dhamira yake ni kuiendeleza Dini ya Kiislamu na kuimarisha maadili mema.
Mkurugenzi wa ZBC Ndg.Ramadhan Bukini ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuridhia na kusaidia kufanyika kwa Mashindano hayo jambo ambalo linadhihirisha Mapenzi ya Viongozi kwa Wananchi wake.
Wadau wa kuhifadhisha Qur- an wakiongozwa na Sheikh Othman Maalim wamewataka Waumini wa Dini ya kKiislam kulipa umuhimu suala la Kuhifadhi Qur-an kwa Vijana wao pamoja na kuisoma kwa wingi hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan .
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mufti kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar yanatarajiwa kufanyikaTarehe 30.03.2024 katika Uwanja wa Amaani Complex Zanzibar na Jumla ya Nchi Nane (8) zinatarajiwa kushiriki katika Mashindano hayo.