Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Sera ya Uchumi wa Buluu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina Dhamira ya kuimarisha uchumi wa Nchi kwa haraka.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Mkoa wa Mjini Magharibi alipozindua duru ya kwanza ya utoaji wa Vitalu kwa Kampuni kwenye maeneo ya Bahari kwa Zanzibar.
Amesema, katika utekelezaji wa dhana ya uchumi wa Buluu, Serikali inatoa fursa kubwa kwa wawekezaji wa sekta ya Mafuta na Gesi asilia na kuwahakikishia Mazingira Rafiki ya utekelezaji wa shughuli hizo.
Hata hivyo Dk. Mwinyi amewahakikishia wawekezaji wote wa Sekta ya Mafuta na Gesi pamoja na Sekta nyengine za uchumi kwamba, Serikali iko tayari kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji kwa Taifa kwa ujumla.
Waziri wa uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman amesema Sekta ya uchumi wa Buluu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni miongoni mwa maeneo Makuu ya vipaumbele vyake.
Hatua mpya ya maendeleo ya Sekta ya Mafuta na Gesi Zanzibar ilianzishwa mwaka 2015 kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Petroli na 21 ya Mwaka 2015 ya Tanzania iliyoiruhusu kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia shughuli za mafuta na Gesi Asilia wenyewe.