Kumekuwa na Ongezeko la matukio ya ajali za kuzama kwa Watoto na hata Watu Wazima mara kwa mara katika Eneo la Forodhani. Eneo hilo linatajwa kuwa na kina kirefu cha Maji na hakuna maelekezo ya Tahadhari.
Hapana shaka kwamba Eneo la Forodhani hapa Zanzibar ni moja ya Maeneo yenye Fukwe safi na haiba si tu kustarehe, lakini ile sura ya Utalii wa Zanzibar. hata hivyo baadhi ya Maeneo ya Fukwe hiii maarufu kwa sasa ni hatarishi hususani kwa Watoto kuogelea ama Mtu asiye na ujuzi wa Kuogelea.
Kamishna Msaidizi wa Kikosi cha Zima Moto na Uokozi, Haji Pandu, amesema kuna umuhimu wa Wazazi na Walezi kuchukua tahadhari pale Watoto wao wanapokwenda kuogelea kwenye Eneo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Makame Khatibu Haji, yeye anasema Serikali tayari imelitambua Eneo la Forodhani kuwa ni hatarishi hususani kwa Watoto Wadogo na kwamba hatua mbalimbali za kuzuia ajali zinachukuliwa.
Tumezungumza na Wavuvi wa Eneo la Forodhani na wao wanaiomba Serikali kuweka Mabango maalumu yanayoonesha wazi kuwa Maeneo ya Tembo Hotel, Hayatti pamoja na Serena ni Maeneo hatarishi na hayapaswi kutumika kwa shughuli za Kuogelea, hususan kwa Watoto Wadogo.
Meneja wa Tembo Hotel, Abdul Azizi Osman, anasema Hoteli hiyo inaendelea kuchukua hatua za makusudi za kuwaondoa Watoto wanaoingia Baharini bila uangalizi wa Wazazi ili kunusuru Maisha yao.
Tahadhari hii ni yenye nia njema katika kulinda maisha ya Watoto wanaopenda kuogelea Eneo hilo.
Eneo la Forodhani bado linabaki ni kitovu cha Utalii wa Zanzibar na atakaye, na Aje!



