Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kufanyika kwa Mkutano wa kutoa Mafunzo ya kuzijengea uwezo Kamati za kuchunguza hesabu za Serikali za Mabunge ya Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADCOPAC) kutasaidia kuchochea kasi ya maendeleo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika ufunguzi wa Mkutano wa Mafunzo kwa Wajumbe na Wataalamu wa Kamati za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Sadcopacambapo amesema Mafunzo hayo yatatoa fursa kwa Wataalamu na Wabunge hao kubadilishana uzoefu na kujifunza Mbinu za kukabiliana na Rushwa na kuongeza uwazi na uwajibikaji kutoka Nchi nyengine za Mataifa ya Afrika hasa Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Aidha amesema Serikali zote Mbili SMT na SMZ zinafanya jitihada kubwa katika kukabiliana na Vitendo vya rushwa na kuhimiza uwazi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuzijengea uwezo Taasisi za umma ziweze kufanyakazi kwa weledi.
Mwenyekiti wa SADCOPAC kutoka Zambia Mhe. Warren Chisha Mwambazi amesema ukanda wa Kusini mwa Afrika unakabiliana na masuala mbalimbali ikiwemo kasoro za kifedha hivyo kupitia mafunzo hayo Wataalamu na kamati za PAC za Nchi Wanachama wa SADCOPAC watapewa Taaluma na mbinu za kukabiliana na Rushwa kwa kuzingatia Ripoti za Afisi za Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali Zanzibar Dkt. Othman Abbas Ali amesema Mkutano huo utasaidia kuongeza fursa za uwekezaji Nchini.
Mkutano huo wa Siku 2 ulioandaliwa na Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar utaleta manufaa mbalimbali Nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Watalii, uwekezaji na kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa yanafanikiwa kwa kiasi kikubwa.