Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe Tabia Maulid Mwita, amesema ni jambo la faraja kuona Kinamama wa Biashara ya Chakula, wameekewa mazingira bora ya kuendesha biashara zao katika hali ya salama.
Akizindua Soko la Mama Lishe Kinyasini, amesema ujenzi wa Soko hilo ni utekelezaji wa ahadi za Rais Dk Hussein Mwinyi, kwa Wajasiriamali na itakuwa imeshatatua kasoro zilizokuwa zikikwamisha uendeshaji wa biashara zao kwa ufanisi.
Katibu Mkuu Afisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na idara maalum za SMZ Issa Mahfoudh Haji, amesema ujenzi wa Masoko manne Mkoa wa Kaskazini Unguja, umelenga kuweka mazingira mazuri ya Kibiashara.
Amesema ujenzi wa Soko la Mama Lishe, umegharimu kiasi cha Shilingi milioni mia tano, lengo ni kutimiza ndoto za wafanyabiashara ya Chakula ili kutoa huduma kwa watu wengi zaidi.
Nae Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Rashid Hadid Rashid, amesema katika jitihada za kuimarisha hali ulinzi na usalama, Serikali ya mkoa itazidisha kasi ya kupiga vita na kupambana na matumizi ya Dawa za Kulevya.