Zanzibar inatarajia kuzindua Mradi wa Historia wa Uwekezaji katika Visiwa vidogo vidogo kwa Kisiwa cha Bawe kilichopo mkoa wa Mjini Magharib, ambao umegharimu kiasi cha Dola Milioni 37.
Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari Katibu Mkuu Wizara Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji, Ndg.Khamis Suleiman Shibu, amesema Uzinduzi huo ni sehemu ya mpango wa kuimarisha Uchumi unatarajiwa kufanyika Juni 15 Mwaka huu.
Amesema azma ya Serikali kuvitangaza Visiwa hivyo vidogo vidogo, katika Mwaka 2021 ni kuongeza fursa za uwekezaji katika Visiwa hivyo kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, hivyo amewaomba Wananchi kuunga mkono kwa kushiriki katika Uzinduzi huo.
Mradi huo unaojulikana kama COCOON-COLLECTION unamilikiwa na Wawekezaji wa Italy na Luxemburg, unatarajiwa kutoa Ajira zipatazo 400 na utazinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Katika hatua nyengine Katibu Shibu, ameipongeza Bodi Mpya ya Wakurugenzi Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ZIPA iliyoteuliwa hivi karibuni.