Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Makumbusho ya Amani na Viumbe hai yatasaidia kukuza Sekta ya Utalii na Uchumi wa Nchi kwa vile ni Kivutio kikubwa cha Wageni wanaoitembelea zanzibar.
Makamu wa Pili ameyasema hayo alipofungua makumbusho ya Amani na Viumbe hai yaliyopo Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar, amesema Serikali imejipanga kufanya matengenezo katika maeneo yote ya Kihistoria ikiwemo Fufuni Pemba, Msikiti wa Kihistoria wa Kichokochwe Pemba, eneo la Kihistoria la Maruhubi, Kijichi, Hamamni na Kizimkazi kwa lengo la kukuza Sekata ya Utalii pamoja kuengeza pato la Nchi.
Aidha Mhe. Hemed amewataka Wafanyakazi wa Makumbusho ya Amani na Viumbe hai pamoja na Makumbusho mengine kuyatunza, huku akikemea uvamizi maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Makumbusho.
Waziri wa Utalii na mambo ya kale Zanzibar Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inahuwisha Sekta ya Utalii na mambo ya kale kwa kuyafungua makumbusho yote ambayo yalikuwa hayafanyi Kazi ndani ya Zanzibar.
Akisoma taarifa ya Kitaalamu juu ya Uzinduzi wa Makumbusho ya Amani na Viumbe Hai, Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya kale Dkt. Aboud Suleiman Jumbe amesema kupitia Mradi wa kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya urithi Serikali imeamua kuyafanyia Marekebisho ili kuyarejesha katika Haiba yake.
Zaidi ya Shilingi Bilioni Saba zimetumika katika matengenezo ya Makumbusho hayo.