Wizara ya Afya Zanzibar imetiliana Saini na UNICEF Mkataba wa Manunuzi wenye Thamani ya Dola Milioni 12 na Laki Tano sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni Thelathini kupitia Mradi wa uwekezaji wa huduma ya Mama na Mtoto unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Kupitia Mkataba huo uliotiwa Saini na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Habiba Hassan Omar na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF Tanzania, lengo kuu la Mradi ni kuimarisha Afya ya uzazi kwa Mama na Mtoto, hivyo pamoja na mambo mengine itahusisha Ununuzi wa Vifaa vya Teknolojia ya mawasiliano vitakavyounganisha vituo vya Afya 52, Vifaa tiba kwa Hospitali za wilaya na Benki ya Damu.
Baada ya utiaji Saini huo Waziri wa Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali itahakikisha Mradi huo unawahusisha kikamilifu Walengwa na utaimarisha Afya ya Uzazi.
Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Tanzania, Elke Wisch pamoja na Mwakilishi wa Benki ya dunia wamesema hakuna Mama wala Mtoto atakaeachwa nyuma kupitia Mradi huo.
Mradi huo unatekelezwa kuanzia Mwaka 2023 hadi 2027.