Benki ya NMB imetanua wigo wa kushiriki katika masoko ya mitaji kimataifa kwa kuiorodhesha hatifungani yake ya jamii (NMB Jamii Bond) jana katika Soko la Hisa la London (LSE).
Hatua hiyo inaifanya NMB kuwa taasisi ya kwanza Tanzania kuwa na hatifungani katika soko hilo kubwa kuliko yote ya hisa duniani na benki ya kwanza Afrika Mashariki, Kati na Kusini kuorodhesha hatifungani ya uendelevu LSE.
Uzinduzi wa mauzo ya Hatifungani ya Jamii ulifanyika wakati wa ufunguzi wa shughuli za wiki hii za LSE, maarufu duniani kwa kuendeleza uwekezaji unaozingatia masuala ya mabadiliko ya tabia, ufadhili wa uendelevu na uwekezaji wa kijani.
Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bi Julia Hoggett, alisema LSE inajivunia kuhusishwa na dhamana hiyo anzilishi ya ufadhili wa uendelevu ya NMB ambayo ni ubunifu mahususi kwa ajili ya kuchochea uwekezaji katika miradi yenye tija kijamii na kimazingira.
Afisa Mtendaji Mkuu Ruth Zaipuna aliyewaongoza maafisa wa NMB kushuhudia tukio hilo alisema uorodheshwaji huo wa kihistoria unaiweka pazuri benki hiyo katika masoko ya fedha duniani na kwenye macho ya jumuiya ya wawekezaji wa kimataifa.
Miongoni mwa waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza, Bw Mbelwa Kairuki na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo wa Uingereza, Bw Andrew Mitchell, ambao uwepo wao ulionesha kuwa kuiorodhesha hatifungani hiyo pia ni jambo jema kidiplomasia.
Jamii Bond ni toleo la kwanza la Waraka wa Matarajio wa Benki ya NMB wa Programu ya Utoaji wa Hatifungani ya Muda wa Kati wa sasa hivi wa miaka 10 wenye thamani ya TZS trillion 1 ambao mapato yake yatatumika kufadhili miradi yenye tija kama nishati mbadala, usalama wa chakula, majengo ya kijani, na kutengeneza ajira.