MAMLAKA YA HIFADHI YA NGONGORO YASEMA HAKUNA MWANANCHI ATAKAYEPATA NYUMBA KINYUME NA UTARATIBU

Ngorongoro

     Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema kwamba ipo makini kuhakikisha kuwa kila kaya inayojiandikisha kuhama kwa hiyari ndani ya hifadhi inapata nyumba katika Kijiji cha Msomera  kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na kwamba hakuna mtu atakayeweza kupata nyumba kwa njia za udanganyifu.

      Akizungumza katika kipindi maalum kilichorushwa na Redio Lumen ya mjini Karatu Mkoani Arusha Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa umma wa mamlaka hiyo Bw. Hamis Dambaya amesema kuna baadhi ya watu wameanza kutafuta njia za uongo ili kupata nyumba jambo ambalo mamlaka imelibaini na kuanza kulifanyia kazi.

       Amesema baadhi ya watu hao ni wale waliohama miaka mingi iliyopita ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na waliposikia kuwa serikali inatoa nyumba kwa kila kaya inayohitaji kuhama baadhi yao wameanza kutafuta njia za kupita ili waweze kupata nyumba kinyume na utaratibu.

       “Kwa ujumla katika zoezi hili serikali kupitia NCAA ipo makini na kila mwananchi anayeishi ndani ya tarafa hii, hakuna mtu yoyote atakayethubutu kupata nyumba kinyume na taratibu kwani taarifa zote muhimu za wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi zipo katika mifumo sahihi”,alisema Bwana Dambaya.

      Kuhusiana na taarifa kwamba baadhi ya watu wanatoka Ngorongoro na kwenda Msomera kutembea na hatimaye kutotaka kurudi Ngorongoro bwana Dambaya amewataka wananchi wanaohitaji kuhama kwa hiyari kufuata taratibu na kuhakikisha hawaendi katika Kijiji cha Msomera mpaka mchakato wa stahikli zao uwe umekamilika.

       “Msomera imekuwa ni Kijiji cha mfano na mvuto kwa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro na baadhi yao inadaiwa wanakwenda huko bila kufuata taratibu, tunawaomba wafuate taratibu na watahamishwa bila shaka yoyote kwa kulipwa stahiki zao,” alisema bwana Dambaya.

 

stories
standard
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.