Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Mbili kwa ajili ya kusafisha Mitaro yote ya kupitishia Maji ya Mvua ili kuepusha kuathiri Makaazi ya Watu na Maeneo mengine.
Akizungumza baada ya kukagua Bwawa la Mwantenga kwa Mtumwa Jeni amesema hatua hiyo itachukuliwa ili kuhakikisha hakuna madhara yanayotokea, hivyo Serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu katika Maeneo ya wazi ili kuondosha kasoro za mafuriko ya Mvua na athari yoyote isitokee kupitia Mradi wa Big-z.
Meneja Miradi wa Usafishaji wa Bwawa la Mwantenga kutoka Manispaa ya Mjini Juma Nassor Harith amesema wamelazimika kulisafisha Bwawa hilo kutokana na athari wanazopata Wananchi katika kipindi cha Mvua na kusababisha Mafuriko ndani ya Makaazi ya Wananchi.
Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji na Operesheni za kimazingira kutoka Idara ya Mazingira Makame Haji Khamis amewaomba Wananchi kuacha kutupa taka ovyo na kutumia sehemu sahihi ili kuepusha athari za kimazingira zinazoweza kuepukika.
Meneja mradi kutoka Kampuni ya CRJE Ndg.Isaya Shija Msafiri ametoa Shukrani kwa Serikali kwa kuiamini Kampuni hiyo na kuahidi kuumaliza Mradi huo kwa wakati uliopangwa.