Uzalishaji wa Mwani katika Kijiji cha Muungoni Wilaya ya Kusini Unguja unatarajiwa kupanda kutoka Tani Kumi hadi 20 kwa kila Bamvua kutokana na Kulima Kitaalamu pamoja na kuwa na Nyenzo za Kisasa zinazorahisisha shughuli hiyo.
Wakaazi wa Kijiji cha Muungoni ambacho mashuhuri kwa Kilimo cha Mwani wakizungumza kufuatia msaada wa Boti waliyopatiwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Mazingira TNC, wameeleza matarajio yao baada ya Boti hiyo ni kuongeza uzalishaji.
Akikabidhi Boti hiyo kwa Wakulima wa Mwani, Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya Uvuvi Dkt. Salum Soud Hamed, amesema sekta ya Uchumi wa Buluu inaendelea kupata mafanikio kutokana na uungwaji Mkono kutoka kwa Washirika wa maendeleo ili kufika matarajio ya kuzalisha Tani elfu 30 kwa Mwaka Nchini.
Mtaalamu Mbobezi wa Kilimo cha Majini kutoka TNC, Ayubu Misheli Singoye, amesema Shirika limekuwa likitoa Elimu ya namna ya kuzalisha Mwani kisasa bila kuathiri mazingira.
Boti hiyo ina thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 30.