Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi imeridhishwa na maendeleo ya Viwanda vya Idara Maalum za SMZ na kueleza kwamba uwekezaji huo utachochea upatikanaji wa Ajira pamoja na kuondokana na uagizaji wa vitu visivyo na ubora Nje ya Nchi.
Wajumbe wa Kamati hiyo Chini ya Mwenyekiti wake Mhe.Machano Othman Said wametoa rai hiyo wakati walipotembelea Kiwanda cha Ushoni wa bidhaa mbali mbali ikiwemo Nguo, Viatu, Uchapaji na Uzalishaji wa mifuko kinachosimamiwa na Idara Maalum za SMZ.
Wameipongeza Idara Maalum ya SMZ kwa kusimamia kwa dhati dhana ya Uchumi wa Viwanda ambao unaweza ukasaidia kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa kutoka Nje.
Mkurugenzi Mtendaji wa Viwanda vya Idara Maalum za SMZ Ndg.Ramadhan Ibrahim akiwasilisha Taarifa ya uzalishaji wa Viwanda hivyo amesema Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha Viwanda ikiwemo kupatiwa Mashine za kisasa kwa matumizi ya kuzalisha bidhaa zilizo bora na zenye kupendwa na Wananchi wa Zanzibar.
Katika hatua nyengine Kamati hiyo ilitembelea katika Miradi ya Kituo cha Daladala Mndo na ujenzi wa Soko la Wajasiriamali kwa kisasi.