Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dtk. Emmanuel John Nchimbi amesema uamuzi wa kuwepo kwa Serikali ya umoja wa Kitaifa Zanzibar ulizingatia usalama wa maisha ya Watu kuliko maslahi ya Vyama vya Siasa.
Dkt. Nchimbi amesema kuwepo Serikali ya umoja wa Kitaifa umeondoa hali ya Siasa za Chuki na Uhasama, huku akisisitiza kuwa Chama cha Mapinduzi kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuongoza kwa misingi ya haki na uwajibikaji ili kudumisha umoja na utulivu Nchini.
Dkt Nchimbi akizungumza na Wazee wa Mikoa minne ya CCM kichama Unguja ikiwa ni Siku ya Pili akiwa kwenye ziara ya Kikazi, akitokea Pemba pia amesisitiza kuendelea kuenziwa Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na umuhimu wake kwenye kuimarisha maendeleo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema CCM inajivunia kwa kuwa na hazina ya wazee wenye Uzalendo, Busara,Hekima na uwezo wa kushauri mambo mambo mbalimbali yenye manufaa kwa maendeleo ya chama na Serikali zake kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar Khadija Jabir, amewasihi Wazee kutumia busara zao kushauri na kutoa maoni ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi na Serikali.