Jamhuri ya Watu wa China imesema Watalii wengi wa China wamehamasika kutembelea Zanzibar kutokana na mandhari iliyopo na Utamaduni wa Asili wa Watu wake.
Akikabidhi Vifaa vya Usafi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe.Masoud Ali Mohammed kwa ajili ya Manispaa ya Mjini, Kaimu Balozi Mdogo wa China aliepo Zanzibar Bw. Zhang Ming, amesema ni jambo la faraja kuona Mji wa Zanzibar unaendelea kuwa safi na kuwa kivutio kwa Wageni wengi zaidi
Kwa upande wake, Waziri Masoud Ali Mohammed, akikabidhi Vifaa hivyo kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, amesema Jamhuri ya Watu wa China imekuwa na uhusiano mzuri na Zanzibar na kuunga mkono jitihada za kimaendeleo ikiwemo za kuimarisha usafi wa Mji.
Amesema kuna Mataifa mengi Washirika Duniani, lakini China imekuwa ni ya kwanza katika kuchangia shughuli za maendeleo, hali ambayo inadhihirisha kuimarika uhusiano wa muda mrefu kati ya Nchi mbili hizo.
Aidha ameitaka Manispaa hiyo kuhakikisha Vifaa hivyo viwe ni sababu ya kuleta mabadiliko ya usafi katika mazingira yetu.
Nae Mstahiki Meya Baraza la Manispaa Mjini Ali Haji Haji, amesema vifaa hivyo ni Mabero na Mapipa ya kuhifadhia Taka vimegharimu zaidi ya Shilingi Milioni Thelathini vitatumika kama ilivyokusudiwa.