Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Norwey inajipanga kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa Nishati ya Umeme utakaokuwa wa uhakika na endelevu Mjini na Vijijini.
Akizungumza katika Kikao cha kupitia matokeo, Maendeleo na hatua mbalimbali zilizochukuliwa baina ya Norwey na Shirika la Umeme Zanzibar kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph Joh'n Kilangi amesema kutokana na upungufu wa umeme unaojitokeza katika maeneo mbalimbali Nchini Serikali imefanya mazungumzo na Norwey kwalengo la kuimarisha utoaji wa huduma hiyo muhimu ya Umeme kwa Wananchi Unguja na Pemba.
Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Khamis Ahmada Fakih amesema tatizo la kukatika kwa Umeme mara kwa mara Nchini linatokana na Miundombinu Chakavu na kuzidiwa na wingi wa matumizi hivyo Mkutano huo na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Umeme kutoka Norway ni miongoni mwa juhudi za kutafuta ufumbuzi wa kutatua tatizo hilo na kuhakikisha kila Mtu ananufaika na matumizi ya Umeme kwa urahisi na ufanisi.
Balozi wa Norway Nchini Tanzania Tone Tinnes amesema Norway itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha Sekta ya Nishati ya Umeme na kuwajengea uwezo Watendaji wa ZECO ili Wananchi wa mjini na Vijijini waweze kunufaika na Nishati hiyo muhimu.