Kufanyika kwa Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za SMT na SMZ kutasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi za Umma Visiwani Zanzibar na tanzania Bara..
Akifungua Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za SMT na SMZ katika kusherehekea Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema Serikali zote Mbili zimeamuwa kuanzisha Mkutano huo ili Wakuu wa Taasisi za Umma waweze kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora za kuimarisha Taasisi hizo ili kuliletea Taifa Maendeleo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la wakuu wa Taasisi Latifa Khamis amesema lengo la mkutano huo ni kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Taasisi hizo kwa kuendeleza umoja wao ili kuibua mbinu mbali mbali zitakazoweza kuleta mafanikio katika Taasisi hizo.
Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya matayarisho ya Mkutano huo Hawwah Ibrahim mbaye amesema miongoni mwa maazimio ya mkutano huo ni pamoja na kuanzisha jukwaa la CEOS, kuendeleza ushirikiano wa kiutendaji na kutatua matatizo madogo madogo zilizobaki kati ya Serikali hizo mbili.
Akifunga mkutano huo Waziri wa Biashara na maendeleo ya Viwanda Mhe Omar Said shaaban ameahidi kutoa ushirikiano katika kufanikisha maazimio ya Jukwaa la Viongozi hao yanayolenga kukuza ushirikiano kati ya jukwaa la SMT na SMZ na kuwasihi Viongozi hao kuendesha majukwaa hayo Kitaaluma.
Mkutano huo wa kwanza wa Wakuu wa Taasisi za SMT na SMZ uliofanyika katika ukumbi wa Dk. Hussein Mwinyi kwenye maonesho ya 10 ya Biashara ya Kimataifa huko Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi umeratibiwa na Wizara ya Biashara na maendeleo ya Viwanda Zanzibar.