Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chaani, Ayoub Mohammed Mahomud ameweka bayana dhamira yake ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi jimboni humo kwa kutangaza kuanza kwa utekelezaji wa ahadi zake nne kuu alizozitoa wakati wa kipindi cha kampeni.
Akizungumza leo na Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kisauni, Mbunge huyo amesisitiza kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni Usalama wa Chakula, akilenga kuhakikisha jimbo hilo linakuwa na akiba ya kutosha ya chakula isiyopungua tani 100 kila mwaka.

“Tuliahidiana mambo manne, na leo tumekuja kuanza utekelezaji wake. Tunataka Chaani iwe na chakula cha kutosha, na ndio maana tumeanza na kundi hili la usalama wa chakula tukishirikiana na SACCOS zetu,” Amesema Ayoub
Aidha Mhe. Ayoub ameelezea neema ya vifaa mbalimbali vya uzalishaji vinavyotarajiwa kuwasili jimboni hivi karibuni, vikiwemo Boti 10 ambapo nne tayari zimeshapatikana, vifaa vya ukulima wa mwani tai-tai, Matrekta mawili makubwa, mashine za kulimia, (power tillers), na ufunguzi wa duka la pembejeo, Ufunguzi wa duka la michezo na utoaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo wadogo.

Naibu Waziri aliweka wazi kiasi cha fedha kilichopo katika mfuko wa jimbo kwa sasa ambazo ni Shilingi Milioni 54 na alifanunua kuwa Milioni 20 zinatoka katika Mfuko wa Mwakilishi na Milioni 34 zinatoka katika Mfuko wa Mbunge.
Sambamba na hilo, Ameahidi wananchi fedha hizo zitatumika kwa uwazi na wananchi wenyewe ndio watakaopanga vipaumbele vya matumizi kulingana na makundi yaliyoelekezwa.

