DKT. MWINYI AHIMIZA VIJANA KUSOMA QUR-AN ILI KUJENGA KIZAZI CHENYE MAADILI

DKT.MWINYI
English

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utaratibu wa kuisoma, kuihifadhi na kuzingatia mafundisho ya Qur-ani Tukufu miongoni mwa Vijana ili kujenga kizazi chenye Maadili, hofu ya Mwenyezi Mungu na mchango mzuri katika Jamii.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Mashindano ya Kitaifa ya Qur-ani Tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aisha Sururu Foundation, yaliyofanyika Jijini Dar es salaam, ambapo Mashindano hayo yamewakutanisha Washiriki kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, yakidhihirisha mshikamano wa Kitaifa na kukuza Vipaji vya Usomaji wa Qurani Nchini.

 

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Waumini kuongeza juhudi katika Ibada ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na kuimarisha matendo ya huruma na ukarimu kwa kuwasaidia Watu wenye uwezo Mdogo, Wajane na Mayatima, akieleza kuwa hatua hiyo huleta Baraka, kuimarisha Mapenzi na kuendeleza amani katika Jamii.

Mwakilishi wa Taasisi ya Aisha Sururu Foundation, amesema Taasisi hiyo inathamini juhudi za Dkt. Mwinyi katika kuunga mkono masuala ya Elimu Nchini.

Mashindano hayo yamejumuisha kuhifadhi Qurani Tukufu kuanzia Juzuu 3, 5,10, 20 na Juzuu 30 kwa Washiriki wa Kike na wa Kiume, pamoja na makundi maalum, ambapo Said Rashid Bakari kutoka Dar es salaam ameibuka Mshindi wa Kwanza katika kipengele cha kuhifadhi Juzuu 30 na kutunukiwa zawadi ya Shilingi Milioni 5.

 

Mashindano pia yaliambatana na utoaji wa tuzo maalum, ambapo kwa heshima na kumbukumbu ya Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Dkt. Mwinyi alipokea tuzo hiyo kwa niaba yake, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuenzi, kuhamasisha na kuendeleza mafundisho ya Qurani Tukufu.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Mama Mariam Mwinyi, Viongozi wa Dini, Wadhamini, Washiriki wa Mashindano pamoja na Wananchi kwa ujumla.

 

Simplenews subscription

The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.