Meneja wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ametia saini mkataba mpya na klabu hiyo utakaodumu hadi Juni 2026.
Muitaliano huyo, mwenye umri wa miaka 64, aliteuliwa Bernabeu kwa mara ya pili mwaka 2021 kwa mkataba wa awali wa miaka mitatu.
Alihusishwa na kuchukua nafasi ya meneja wa Brazil mapema mwaka huu lakini akasema anataka kubaki katika klabu hiyo.
Ancelotti ameshinda mataji 10 kama kocha wa Real, yakiwemo mawili ya Ligi ya Mabingwa - hivi karibuni katika msimu wake wa kwanza akiwa na klabu hiyo mnamo 2021-22.
Pia amebeba taji moja la La Liga, Copas del Rey mawili, Vikombe viwili vya Dunia vya Klabu, Vikombe viwili vya Uropa na Super Cup mara moja.
Hapo awali Ancelotti aliiongoza Real kati ya 2013 na 2015, na kuondoka kwake kulikuja mwaka mmoja baada ya kushinda Ligi ya Mabingwa.
Alirejea kwa kipindi cha pili, akichukua nafasi ya Zinedine Zidane, baada ya kuondoka katika klabu ya Ligi ya Premia ya Everton mnamo Juni 2021.
Kocha huyo wa Real ndiye kocha pekee aliyeshinda vikombe vinne vya Uropa, huku akiwa wa kwanza kushinda ligi kuu tano za Ulaya nchini Italia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Uhispania.
Msimu uliopita, Real walishinda Copa del Rey lakini walimaliza washindi wa pili mbele ya Barcelona katika ligi kuu ya Uhispania na kutoka katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Msimu huu, wanaongoza La Liga baada ya mechi 18 na kusalia katika mashindano yao yote ya kombe la Ulaya na la nyumbani.