Shirika la Bima Zanzibar ZIC likishirikina na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Fondation wamekabidhi msaada wa Vitabu vya Mitaala kwa Skuli za Secondari ili kukuza kiwango cha ufaulu katika Skuli za Mkoa ya Kusini Unguja.
Akikabidhi Vitabu vya Mitaala kwa Skuli za Sekondari, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Bima Zanzibar Ndg.Jape Ussi Khamis amesema Elimu ndio msingi wa maendeleo katika Nchi hivyo ni vyema kwa Jamii kuunga Mkono jitihada za Serikali katika kuendeleza upatikanaji wa Elimu bora.
Amesema Shirika la Bima litaendelea kushirikiana na Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ili kuona malengo ya kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini yanafanikiwa kwa kukuza Kiwango cha Ufaulu kwa Wanafunzi.
Mkurugenzi Mtendaji Sabra Mohamed kutoka Mwanawake Initiatives Fondation amesema moja ya Vipaumbele vya Taasisi hiyo ni kuhakikisha wanasaidia jitihada za upatikanaji wa Elimu bora kwa kuweka Miundombinu imara na endelevu kwa Vijana ili waweze kufikia malengo yao na Taifa kwa Ujumla.
Afisa huduma za Wanafunzi Idara ya Elimu Sekondari Bi.Rukia Ramadhani amesema Wizara ya Elimu bado inahitji Vitabu kwa Maendeleo ya Wanafunzi hivyo amewataka Wadau kuendelea kuchangia ili kukuza Maendelo ya Elimu Nchini.