Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na Mshirika ya Kimataifa na Wadau wengine kuhakikisha kuwa Maradhi ya Malaria yanaondoka hapa Nchini.
Akifungua Mkutano wa Mpango kazi kwa Mwaka 2025 uliowashirikisha Wadau na Mashirika ya Kimataifa Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim amesema juhudi zinafanyika kwa Wananchi juu ya kujikinga na Maradhi hayo ambapo katika kipindi cha Miaka Ishirini nyuma Zanzibar iliweza kudhibiti Maradhi ya Malaria kwa kiasi kikubwa, hata hivyo katika kipindi cha hivi karibuni kulitokea mripuko wa Maradhi hayo yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia Nchi.
Meneja wa Programu ya kumaliza Malaria Zanzibar Shija Joseph Shija amesema lengo la Mkutano huo ni kuwakutanisha Wadau wanaosaidia mapambano dhidi ya Malaria na kuandaa mpango kazi wa Mwaka mmoja na kuwasilisha na kuweza kuidhinishiwa Fedha kwa ajili ya matumizi.
Katibu Mtendaji wa kupambana na Maradhi ya Malaria Kifua Kikuu na Ukimwi katika Ofisi ya makamo wa Pili wa Rais Dkt Abdalla Suleiman amesema kazi kubwa wanayoifanya ni kusaidia katika kutafuta Fedha, Wataalamu ili kuendeleza kazi kwa mujibu wa muda uliopangwa.
Mkurugenzi anaeshughulikia masuala ya Afya USAID Anne Murphy amesema wamesaidia Nchi mbali mbali ikiwemo Tanzania, Kenya Uganda katika mapambano dhidi ya Malaria na kupatikana kwa mafanikio makubwa.