WAZIRI PEMBE ASISITIZA JUU YA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA WASICHANA ILI KUWAKINGA NA MIMBA ZA UMRI MDOGO PAMOJA NA MAAMBUKIZI YA MARADHI MBALIMBALI

Waziri Pembe

    Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana ili kuwaepusha na mimba za umri mdogo pamoja na maambukizi ya maradhi mbalimbali.

     Akizungumza katika sherehe ya siku ya Hedhi Salama Duniani, iliyoadhimishwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya WAJAMAMA na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, huko Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, amesema afya ya uzazi kwa wasichana ni muhimu kwani inawasaidia kujitambua na kuepukana na vishawishi.

    Amesema siku ya Hedhi Salama ni siku muhimu kwani inasaidia katika kupeana elimu juu ya namna ya matumizi bora ya taulo za kike pamoja na namna ya kujisafisha kwa wasichana na akina mama.

   Aidha amewataka Wanafunzi walioshiriki maadhimisho hayo na kupewa elimu kutambua kuwa suala la hedhi ni hali ya kawaida kwa mwanamke na ni suala la kimaumbile kwani hata katika dini limetajwa, hivyo amewataka kutokuwa na huzuni na kujiamini na kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao.

   Pia amewataka kujitambua na kuridhika na hali walizokuwa nazo kwani kuna vishawishi vingi vinavypelekea udhalilishaji hali ambayo itawasababishia kupoteza utu wao.

    Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJAMAMA Ndugu Nafisa Jidawi amewataka kutambua kuwa wanapopatwa na siku zao za hedhi hawatakiwi kupata maumivu hivyo ikiwatokea hali hiyo wanatakiwa kuonana na wataalamu wa afya ili waweze kupatiwa matibabu ya haraka.

    Kwa upande wake Ndugu Fatma Fungo Kutoka Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation amesema Takwimu zinaonesha kuwa siku 48 wasichana wengi wanakosa kuwepo skuli kutokana na kupata maumivu wakati wa hedhi, ambapo hali hiyo inapelekea kuwepo kwa hali ya utoro mashuleni, kudhoofika kwa afya na afya ya uzazi kuathirika, hivyo amesema kuna umuhimu wa kutafuta ufumbuzi ili kuweza kupunguza changamoto hizo.

 

stories
standard
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.