Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameitaka jamii kulipa mkazo suala la unyonyeshaji wa ziwa la mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ili kuwakinga watoto na aina zote za utapiamlo unaojumuisha matatizo ya upungufu wa virutubishi mwilini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika wiki ya unyonyeshaji huko Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Unguja alisema kuna baadhi ya jamii zinazoamini kumyonyesha mtoto ziwa la mama pekee kunaweza kuleta athari mbalimbali kwa mama na mtoto jambo ambalo sio sahihi, hivyo aliwataka akina mama kupuuza dhana potofu za unyonyeshaji katika kipindi hicho na badala yake kuendelea kuwanyonyesha watoto kwani ni msingi wa afya bora kwao.
Alisema kuna faida mbalimbali zinazopatikana endapo mtoto atanyonya maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo ikiwa ni pamoja na kumpatia mtoto kinga dhidi ya maradhi mbalimbali, kuleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto pamoja na kumfanya mtoto kuwa na afya nzuri ya mwili na akili.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 za unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee zinaonesha kuwa bado Zanzibar kuna kundi kubwa la watoto wanaolishwa chakula mbadala wa maziwa ya mama chini ya miezi sita ,jambo ambalo alilitaja kuwaweka hatarini zaidi watoto hao kupata uzito uliozidi na kupata kiribatumbo.
Hivyo alisema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, wadau na asasi za kiraia ili kuwasaidia wanawake kuondokana na vikwazo na kutatua changamoto zinazowakabili katika kufanikisha unyonyeshaji.
Alifahamisha kuwa hali nzuri ya lishe ya mama mjamzito humsaidia kuufanya mwili wa mama kuwa na hifadhi ya kutosha ya tabaka la mafuta na kujiandaa vyema kwa unyonyeshaji mara baada ya kujifungua.
Kwa upande wake Mkuu wa UNICEF Ofisi ya Zanzibar, Laaxmi Bhawani alisema licha ya kuwa tafiti zinaonesha kuwa mtoto anaenyonyeshwa maziwa ya mama pekee ana hatari ndogo ya magonjwa na kifo katika miezi sita ya mwanzo ukilinganisa na mtoto asienyonyeshwa lakini bado mwamko wa unyonyeshaji katika kipindi hicho kwa upande wa Zanzibar ni mdogo ambapo takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa asilimia 40 ya watoto ndio wanaonyonyeshwa ziwa la mama pekee.