Jeshi la Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa Mifugo kimesema hakuna sheria inayomruhusu mtu yoyote kujichukulia sheria Mkononi huku likibainisha kuwa tayari linayomajina ya watu waliojichukulia sheria Mkononi na kubomoa nyumba na kuchukua mifugo ya wakazi wa Engikaret Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha.
Hayo yamesemwa leo Aprili 25,2024 Wilayani Longido Mkoani Arusha na Kamanda wa Polisi Kikosi cha kuzuia wizi wa Mifugo Nchini Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Engikaret ambapo amewambia Jeshi hilo kwa kushirikiana na viongozi wengine watahakikisha hakuna mwananchi ambae ananyanyaswa wala kuchukuliwa mifugo yake.
Ameongeza kuwa hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kujichukulia hatua na kuvunja ama kupiga wafugaji ambapo amesema kikosi hicho kitashirikina na viongozi wa eneo hilo ili kuwabaini watu wengine waliohusika katika kuvunja na kuchukua mifugo katika Kijiji cha Engikaret Wilayani Longido Mkoa wa Arusha.
Kamanda Pasua amesema watu wote waliohusika katika uhalibifu wa mali na kuiba mifugo ya wananchi watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili wakajibu tuhuma zinazowakabili huku akiwaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwabaini watu ambao wanachafua taswira nzuri ya jamii ya kimasai.
Elia Lukumay ambae ni mkazi wa Engikaret Longido amesema kuwa wao hawajawahi kufanya vurugu wala kuiba mifugo huku akibainisha kuwa wanaliomba Jeshi la Polisi kuendelea kushirikkna na Jamii hiyo ili kuwaibaini wale wote waliohusika katika tukio hilo.
Nae Christopher Lemaliga amesema viongozi wanapaswa kuendelea kuwasikiliza wananchi ambao wanachangamoto huku akiwaomba viongozi wanaofika katika maeneo yenye changamoto kukutana na viongozi wenyeji ili kumaliza changamoto zilizopo.