Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba kuhakikisha Ujenzi wa bustani ya Mwanamashungi unakamilika kwa kipindi Kifupi ili kutoa nafasi kwa Wananchi kulitumia eneo hilo.
Akikagua Maendeleo ya Ujenzi wa Bustani hiyo Mhe Hemed amesema kuna uhaba wa maeneo ya kupumzukia kwa wakaazi wa maeneo hayo na maeneo Jirani ya Chake Chake hivyo Baraza la Manispaa wanalazimika kuchukua juhudi kuhakikisha mkandarasi anamaliza Ujenzi huo kwa wakati na Viwango vinavyotakiwa ili wananchi waweze kunufaika na Bustani hiyo huku akitaka kuwekewa uzio eneo linalozunguka Bustani hio kwa ajili ya usalama wa Wananchi.
Wakati huo huo mhe Hemed amekagua Ujenzi wa Maegesho ya Magari pamoja na Ujenzi wa Nyumba za Makaazi na Maduka zinazojengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar katika eneo la Mabatini Chake Chake ambapo amesema Miradi yote inayojengwa na Serikali ina Maslahi kwa Wananchi kwani kukamilika kwa Ujenzi wa Nyumba hizo kutapunguza tatizo la Makazi kwa Wananchi na Wafanyabiasha kufanya Biashara zao katika maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Salha Mohamed Mwinjuma amesema wizara itasimamia na kuhakikisha ujenzi wa Nyumba hizo uliojumiisha na Nyumba za Makaazi na milango ya Maduka unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Mbunge wa Jimbo la Chake - Chake Mhe. Ramadhan Suleiman Ramadhan amesema kukamilika kwa Ujenzi wa Mradi wa bustani ya Mwanamashungi na Miradi mengine kutaubadilisha Muonekano wa mji wa Chake Chake na Wananchi watapata fursa ya kufanya Biashara zao katika eneo hilo.