Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inathamini mchango wa Fani za Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji kwenye utekelezaji wa Mipango mikubwa ya Maendeleo hasa Miradi ya Ujenzi.
Akizindua Taasisi ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar huko Hoteli Verde, Mtoni amesema Serikali itaendelea kuwahusisha kikamilifu kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa kuzingatia dhana ya ushirikishwaji wa Wataalamu Wazawa katika Miradi endelevu ya kimkakati ya uwekezaji Nchini.
Amesema, kwa kiasi kikubwa Serikali imejitahidi kuzitumia Kampuni za ndani kwenye utekelezaji wa Miradi mbalimbali hasa ya Fedha za UVICO kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wapate miradi mikubwa zaidi.
Hivyo Dk.Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali ya Zanzibar chini ya dhana ya Uchumi wa Buluu imeendeleza Sera ya kuajiri Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Wazalendo ikiamini kuwa wana uwezo mkubwa wa kuleta ufanisi mkubwa.
Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Dk.Khalid Salum Mohammed amesema kuundwa kwa Taasisi ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar ni kielelezo muhimu cha kukuza uwezo wao katika kuimarisha Sekta ya Ujenzi kwa Maendelo ya Nchi.
Rais wa Taasisi ya Wasanifu Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar Mhandisi Abduswamad Mohamed Mattar amesema Taasisi hiyo ilimedhamiri kufanya makubwa zaidi kama mchango wao kwa Taifa huku akiwashauri Wataalamu wa Fani hizo kuwa Mashirikiano.