WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua studio za kidijiti za redio ikiwa ni sehemu ya mradi wa maboresho ya studio za redio, televisheni na mitandao ya kijamii za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Amezindua studio hizo za kisasa (Jumamosi, Aprili 20, 2024) kwenye hafla iliyofanyika kwenye studio za shirika hilo, barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Nimefurahi sana baada ya kujulishwa kuwa uzinduzi wa mradi huu umezingatia awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026). Mpango huo umeainisha vipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa usikivu wa redio, ununuzi wa mitambo na vifaa vya redio na televisheni.”
Akiwa kwenye studio hizo, Waziri Mkuu alikagua studio za kisasa na kufanyiwa mahojiano mafupi kwenye studio ya TBC Taifa ambako alieleza jinsi alivyofanyiwa usaili wa kazi ya utangazaji mwaka 1994.
Waziri Mkuu amesema alifanikiwa kupata kazi hiyo lakini kabla hajaripoti akawa amechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Nilitakiwa kuanza kazi Julai 10, 1994 lakini matokeo ya kwenda Chuo Kikuu yakatoka mwezi Juni. Wazee wakanishauri nikasome kwanza, nikimaliza nitakuja kuomba kazi, lakini baada ya chuo, nikaishia hukooo.”
Pia alitembelea studio za TBC International na Bongo FM ambako alikuta vijana ndiyo wanashika usukani wa kuendesha mitambo na vipindi na kuelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Redio, Bi. Aisha Dachi kwamba maudhui yake yamewalenga zaidi vijana.
Naye, Waziri ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mafanikio hayo yote yanatokana na utashi wa kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuamua kuwekeza kwenye shirika hilo.