Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inakusudia kuanzisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu yenye lengo la kutoa fursa za Mikopo kwa Wanafunzi wa Kizanzibari wenye sifa za kujiunga na Masomo Ngazi mbali mbali za Elimu ya juu Ndani na Nje ya Nchi.
Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Leila Muhammed Mussa amesema hayo Wakati akiwasilisha Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, Namba 3 ya Mwaka 2011 na kutunga Sheria hiyo ili kutoa msaada wa kifedha kwa Wanafunzi na mambo mengine , huko katika Baraza la Wawakilishi chukwani ,Amesema hali hiyo italeta muongozo mzuri kwa Wanafunzi katika masomo yao.
Mhe.Leila amesema kwa kuzingatia msingi wa uhitaji wa Wataalamu katika Ngazi mbali mbali za Elimu, Mswada umeweka masharti ya kuipa Bodi ya Mikopo uwezo wa kutoa Mikopo kwa Ngazi ya Stashahada katika Fani za kipaumbele kwa kuzingatia maslahi ya Umma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii Mhe. Sabiha Filfil akitoa maoni ya Kamati ameiomba Wizara ya Elimu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu kuwa anaestahiki kupewa Mkopo wafanye tahfifu wanufaika wa Mkopo kwa Ngazi ya Stashahada na Shahada, ukizingatia wengi wao wanatokana na Familia duni .
Wakichangia mswada huo Wajumbe wameitaka Bodi kuwapatia Wanafunzi hao Fedha hizo kwa wakati ili kuwapunguzia usumbufu kwa Wanafunzi wanapokuwa Chuoni.
Mapema akijibu swali kuhusu ahadi ya Rais juu ya Nauli za Wafanyakazi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema tayari agizo hilo limeshafanyiwa kazi na Afisi kuu ya Utumishi wa Umma na kuliwasilisha Wizira ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kulizingatia katika Bajeti.