Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza juhudi za kuiimarisha Taasisi ya Viwango Zanzibar ZBS kwa lengo la kuinusuru Zanzibar kuwa Jaa la uingiaji wa Bidhaa hafifu na zisizo na Viwango.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema hayo wakati akizungumza katika Uzinduzi wa Kituo kipya cha Ukaguzi wa Vyombo vya Moto kilicho chini ya ZBS Maruhubi chenye uwezo wa kukagua Gari Mia Tatu kwa Siku kwa kutumia Teknolojia ya Kisasa.
Amesema Zanzibar kwa Muda mrefu imekuwa ikibeba mizigo ya bidhaa ziziso na ubora wa Viwango kunakosababishwa na kutokuwepo kwa Kituo cha aina hiyo.
Ameielezea hatua hiyo kuwa itawezesha kulinda afya za Wananchi, uhifadhi wa mazingira ya Nchi na kuweka ushindani wezeshi wa ufanyaji wa Biashara Nchini na kuwataka Watendaji wa ZBS kuitunza Mitambo ya Kituo hicho na kufanya kazi Kitaalamu kufikia malengo ya kuwepo kwa Kituo hicho.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mh.Omar Said Shaaban amesema Takwimu zainaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la uingiaji wa Vyombo vya Moto Nchini hivyo ni vyema kuimarishwa kwa Ukaguzi ili kuwe na usalama wa Nchi.
Akitoa Taarifa ya Kitaalamu juu ya Ujenzi wa Kituo hicho kilichogharimu kiasi cha Shillingi Billioni Moja na Milioni Sabini na Nne Mkurugenzi wa ZBS Ndg.yussuf Majid Nassor amesema Kituo kitafanya kazi kwa saa Ishirini na Nne na kuwasisitiza Wananchi kutohofia kupeleka Vyombo vya Moto kwa ajili ya Ukaguzi.
Kituo hicho cha kisasa kitakachotumia Mfumo wa kisasa kimejengwa na Kampuni ya Kecla Company Limited kwa kushirikiana na Wahandisi wa ZBS .