Akizingumza na Viongozi na Wachezaji wa Timu hizo katika Hafla ya Chakula cha Usiku kilichoandaliwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Viwanja vya Hotel ya Verde Mtoni Zanzibar.
Amesema Serikali inathamini uhusiano unaofanyika baina ya Taasisi, Jumuia na Vilabu vya Michezo kwa pande zote za Muungano kutokana na mchango mkubwa wa kimaendeleo unaopatikana kupitia Mashirikiano hayo.
Aidha Mhe.Hemed amewataka wenye Viti wa Timu hizo Mbili kuendelea kuwaongoza vizuri Wanachama wao na kuhakikisha wanauendeleza umoja wao ambao una mchango mkubwa katika kuimarisha na kudumisha Muungano uliotimiza Miaka Sitini(60) tangu kuasisiwa kwake.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid amepongza uhusiano wao uliodumu kwa muda mrefu ambao umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa pande zote mbili.
Mwenyekiti Mwenza kutoka Timu ya Arusha Wazee Club Ndugu Ally Mamuya amesema ushirikiano kati ya Timu hizo Mbili umekuwa ni wa muda mrefu ambao umekuwa na faida nyingi ikiwa ni pamoja na kufanya Mazoezi ya pamoja kwa kuimarisha Afya ya Mwili na Akili pamoja na kuzidi kuendelea kuutangaza Utalii kati ya Zanzibar na Arusha.
Nae Mwenyekiti wa Timu ya Baraza la Wawakilishi Sports Club Mhe.Miraji Khamis Mussa (Kwaza) ametoa shukran kwa Mabenki mbali mbali hapa Nchini kwa kuwapatia ushirikiano mkubwa katika kufanikisha shughuli mbali mbali za Baraza la Wawakilishi ikiwemo suala zima la Michezo ambalo huwajenga zaidi kiafya.