Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Skuli ya Sekondari Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamra shamra ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema lengo la Serikali ni kutatua tatizo la nafasi katika Skuli za maandalizi, Msingi na Sekondari ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia Watoto kutembea masafa marefu kutafuta huduma ya Elimu.
Mhe. Hemed amesema Serikali inaimarisha Vyuo vya Mafunzo ya Amali kila Wilaya ili kutoa fursa kwa Vijana kujiunga katika Vyuo hivyo, ambapo kwa sasa Serikali imo katika mchakato wa ujenzi wa Vyuo vitano (5) vitakavyowasaidia wananchi kuweza kujiajiri pindi watakapo maliza masomo yao.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Ali Abdulghulam Hussein, amewataka Walimu, Wanafunzi na Wananchi kuwakemea vikali wale wote wanaoyadharau na kuyabeza Mapinduzi na badala yake wawe mstari wa mbele katika kuelimishana juu ya umuhimu wa Mapinduzi kwa kizazi kijacho.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Skuli hiyo kutatoa nafasi kwa Wanafunzi kuingia Skuli kwa muda wa asubuhi na kupunguza msongamano wa Wanafunzi Madarasani ambapo kila Darasa litachukua wastani wa Wanafunzi 45 tu.