Kufuatia tukio la kujeruhiwa kwa kijana Kazungu Julius mtoto wa miaka 10 mwenye Ualbino siku 8 zilizopita katika Kitongoji cha Mtakuja, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, Mkoani Geita Serikali imeingilia kati kukemea vikali vitendo hivyo kwa kuhakikisha aliyetekeza tukio hilo anatiwa nguvuni.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akimuwakilisha Waziri wa Nchi, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Serikali ina mkono mrefu kwahiyo wananchi wawe na amani huku akiahidi kusomeshwa kwa mtoto huyo na kuisihi jamii kuwa na upendo.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Mji Geita Dkt. Stephen Mwaisobwa amethibitisha kuendelea vizuri kwa mtoto huyo na anatarajiwa kuruhusiwa.
Mwenyekiti Taifa wa watu wenye Ualbino Tanzania Bw. Godson Molleli amekemea ukatili huo na kuiomba jamii kuachana na vitendo hivyo na kuahidi kuwa bega kwa bega na familia ya mtoto Kazungu.
Mnamo tarehe 2 mwezi huu majira ya saa mbili usiku tukio la kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali (Panga) lilitendeka kwa mtoto mwenye Ualbino Kazungu Julius anayeishi na wazazi wake, huku aliyetekeleza tukio hilo akitokomea kusikojulikana.
Jeshi la Polisi mkoa wa Geita linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.