Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa amesema Serikali itahakikisha Wananchi wa Mkoa huo wanaendelea kuishi pamoja licha ya tofauti zao za imani ya Dini.
Akizungumza na Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Askofu Augustine Shao wakati alipofika katika Kanisa hilo huko Forodhani, kufuatia tukio lililotokea Mwishoni mwa Wiki iliyopita la kuvunja baadhi ya Masanamu amesema kuwa Serikali ya Mkoa imeguswa na tukio hilo na Serikali itaendelea kuchukuwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu ziliopo.
Kitwana amewahimiza Wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi kuendelea kuheshimu Dini ya kila mmoja ili Jamii iweze kuendelea kuishi kwa amani na utulivu.
Askofu wa Kanisa Katokili Zanzibar Augustine Shao amesema wanaimani kuwa Serikaali italifanyia kazi suala hilo kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi Cleophace Magesa amesema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna watu wengine wanaohusika na tukio hilo.