Mkuu wa Mkoa wa Lindi ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha zinafufua au kuunda madawati ya ulinzi ya watoto sambamba na kuunda klabu za watoto mashuleni zitakazowasaidia kuelezea na kutatua changamoto zao
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa huko katika kijiji cha chienjele halmashauri ya Ruangwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi , Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawale amesema vyombo hivyo ni muhimu kwa ajili ya kutetea maslahi yao pindi watoto wanapokuwa wamefanyiwa ukatili.
Amesema ili Taifa liweze kuendelea kupiga hatua ni muhimu kutilia maanani mahitaji ya watoto ikiwa pamoja na watoto masikini , walemavu na walio na mazingira magumu zaidi kutengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za Halmashauri.
Hata hivyo ameendelea kuikumbusha Jamii kuwa inawajibu wa kutoa taarifa na ushahidi kuhusu mtoto ambae haki zake zinakiukwa na wazazi na walezi au ndugu yoyote kwenye serikali za mitaa na kwenye vyombo vya dola kwa vitendo vya ulawiti, ubakaji na ukatili wanaofanyiwa watoto ili serikali ichukue hatua na adhabu zitolewe.
Akitoa salamu za Wilaya ya Ruangwa Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Ngoma amesema siku hiyo ya Mtoto wa Afrika ni muhimu kwa Nchi za Afrika kutathimini na kueleza Dunia mabadiliko Makubwa yaliyofanywa na Nchi hizo Katika kuwapambania watoto hao Katika kuondoa changamoto mbalimbali ikiwa pamoja na ubaguzi wa rangi unyanyapaa Elimu na kadhalika
Awali afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Lindi ndugu Charles Kigahe alieleza changamoto kadhaa zinazowakabili watoto wa Mkoa huo wa Lindi
Miongoni changamoto hizo ni pamoja na Watoto kutotimiziwa haki ya kupata elimu, hii imetokana na wazazi kutoona umuhimu wa kuwafuatilia watoto pindi wakiwa shuleni ambapo imesababisha watoto kuacha shule.
Watoto kukosa malezi ya wazazi, hii imetokana na wazazi kutengana ambapo mtoto anaendelea kulelewa na mzazi mmoja au bibi. Watoto kukosa mahitaji ya msingi kwa sababu ya kutoelewana kwa wazazi, Watoto kufanyiwa ukatili wa kingono.