Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka tume ya Ulinzi wa taarifa Binafsi Tanzania (PDPC) kuhakikisha ifikapo Disemba Mwaka huu iwe imezisajili Taasisi zote za Umma na Binafsi zinazohusika na ukusanyaji na uchakataji wa Taarifa na kuzisimamia kwenye kutekeleza sheria ya ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Dkt. Samia ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Jijini Dar Es Salaam pamoja na mambo mengine ame ameitaka Wizara ya Habari kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu kazi za Tume ili malalamiko yanayoibuliwa yashughuliwe kwa haki, na kutunza Faragha za Mtu Binafsi kwa Tanzania Bara na Visiwani ili kudhibiti ukusanyaji wa uchakataji wa Taarifa.
Aidha dkt. Samia Suluhu amemuelekeza Waziri wa habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa kazi za Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mara mbili kwa Mwaka, ili kujua mwenendo wa Tume hiyo iliyoanzishwa kwa lengo la kusimamia sheria ya ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyoanza kutumika Rasmi Mei 1, 2023.
Kwa upande wake, waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, nape nnauye amesema kuwa uzinduzi wa tume hiyo na uwepo wa sheria yake ni jambo lenye msingi kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ambazo ni ushahidi kuwa CCM inaamini katika Utu, Ustaarabu na Faragha za Watu, hili linaongeza idadi ya ahadi kubwa ambazo Rais Samia amezisimamia katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa Wananchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (PDPC), Emmanuel Mkilia, amesema Tume hiyo itafanya kazi kwa weledi na kuzingatia umuhimu wa ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa Ustawi wa Maendeleo ya Taifa na kuongeza Ushirikiano Kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya PDPC, takribani Nchi 36 kati ya 54 za Afrika zimetunga Sheria ya Ulinzi wa taarifa Binafsi ambapo kwa Afrika Mashariki Nchi tano kati ya saba zimeshatunga sheria hiyo, huku ikitajwa ni muhimu hasa katika uchumi wa Kidigitali kutokana na ukuaji wa Teknolojia Taarifa za Mtu Binafsi ni muhimu na zimekuwa zikitumika kupitia Mifumo ya Jamii Namba, Anuani za Makazi na Mfumo Jumuishi wa kufanya malipo Mtandaoni.