MBULU MJI YAJIPANGA KUUPOKEA MWENGE WA UHURU 2026 KWA MAFANIKIO

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi. Rehema Bwasi
English

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi. Rehema Bwasi  jana Aprili 1, 2026 ameongoza kikao cha tathmini ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2025, akiwapongeza watumishi wote wa halmashauri hiyo kwa ushiriki wao mkubwa ulioleta mafanikio ya kihistoria.

Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Rehema  alieleza kuridhishwa na namna watumishi walivyojitoa kwa umoja na mshikamano katika kuhakikisha mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yanafanyika kwa ufanisi mkubwa, hali iliyochangia Halmashauri ya Mji wa Mbulu kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika mashindano ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.

“Ushindi huu ni matokeo ya juhudi zenu, nidhamu kazini, na ushirikiano wenu. Mmeonesha mfano wa kuigwa kwa halmashauri nyingine,” alisema Bi.Rehema
 

Aidha, aliwataka Wakuu wa Idara na Vitengo kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza mafanikio hayo kwa kuanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2026, akisisitiza umuhimu wa ubunifu, uwajibikaji, na ushirikiano endelevu.

Bi. Rehema aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana hayapaswi kuwa mwisho bali ni chachu ya kufanya vizuri zaidi mwaka huu, huku akihimiza kila idara kuweka mikakati madhubuti itakayoboresha zaidi utendaji kazi.


 

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa kikao hicho walieleza dhamira yao ya kuendeleza mafanikio hayo kwa kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika mashindano ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2025, jambo linalodhihirisha kiwango cha juu cha maandalizi, usimamizi, na ushirikiano wa watumishi wake.

 

Simplenews subscription

The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.