Mkuu wa Jeshi la Polisi amesema vituo tiba vitaendelea kuboreshwa katika eneo la miundombinu, vifaa tiba na kuwekeza katika raslimali watu ikiwemo kuajiri wataalamu wapya wa Afya.
IGP Wambura ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akifungua mkutano wa Wakuu wa vituo tiba, Wahasibu na Watendaji wa Kikosi cha Afya.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA hivyo amewataka kuwa wepesi katika kujifunza na kutumia mifumo iliyopo ili kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje wanaopata huduma katika hospitali za Polisi.
Aidha, amewataka watendaji wa kikosi hicho kufanya tathmini ya magonjwa mbalimbali ili kurahisha kujua hatua za kuchukua katika kuboresha Afya za Askari na familia zao ikiwemo kusaidia Kamisheni ya Polisi ya Jamii katika kuwafikia wananchi ili kutimiza lengo la Jeshi la Polisi ambalo ni kuzuia uhalifu kabla haujatokea.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Afya, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Lucas Mkondya amesema kikao hicho kinalenga kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa na kikosi hicho ambapo amesema kwa sasa wamejipanga kwenda kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuboresha huduma zaidi zinazotolewa na Hospitali za Polisi baada ya kupatiwa fedha na Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema katika uongozi wa IGP Camillus Wambura kumekuwepo na mafanikio mbalimbali ikiwemo maboresho ya majengo na Vifaa tiba jambo ambalo limefanya huduma kuwa bora katika hospitali za Polisi.
Aidha, alisema wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa Askari Polisi na wananchi wanapata huduma bora.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala ndani ya Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Anthony Ruta alisema huduma bora za Afya kwa Askari na familia za ni nguzo muhimu katika ufanisi wa kazi za Polisi.


