Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Abdallah amewataka Wakandarasi wanaojenga Miradi ya maendeleo kuheshimu Mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na Kampuni husika.
Akizungumza katika Ziara ya kutembelea na kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Maisara Mhe. Hemed amesema baadhi ya Wakandarasi huchelewesha kumaliza Miradi kwa wakati na kuomba kuongezewa muda jambo ambalo linakwamisha adhma ya Serikali ya kutatua kero za Wananchi kwa wakati.
Idha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuanzia sasa Wakala wa majengo Zanzibar (ZBA) wanapaswa kuwachukulia hatua Kampuni yoyote ambayo haitokabidhi Miradi kwa wakati uliopangwa ili iwe fundisho kwa Kampuni nyengine zinazoendelea na Ujenzi wa Miradi mbali mbali Nchini.
Mkandarasi kutoka Kampuni ya china Railway Jianhuwang Engineering (CRJE) Chey Yur amesema licha ya kukabiliwa na matatizo mbali mbali mwanzoni mwa UJenzi huo watahakikisha wanakamilisha na kukabidhi Jengo hilo ndani ya muda waliokubaliana.
Msimamizi wa Majengo kutoka (ZBA) Mohamed Nahoda Mohamed amesema ZBA wanashirikiana kwa karibu na Mkandarasi wa ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 20% ya Ujenzi na wanatarajia kukamilisha mwishoni mwa Mwezi Disemba Mwaka huu.
Ujenzi huo wa jengo la Ghorofa 4 la Ofisi kuu ya Tume ya uchaguzi Zanzibar utakapokamilika utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 11 ambao utajumuisha Ofisi, kumbi za mikutano na Vyumba kwa ajili ya Wageni.