Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni inayotoa huduma za bima zinazozingatia misingi na sharia ZIC Takaful Ndg.Said Abdallah Basleym amesema suala la Mafunzo kwa Wafanyakazi ni jambo la kupewa kipaumbele ili kuhakikisha wanaendana na kasi ya utendaji na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo yaliyotolewa kwa Wafanyakazi wa Kampuni hiyo, Ndg. Said ameeleza kuwa uwekezaji katika Mafunzo husaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Kampuni, pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa Wananchi.
Mada kuhusu maadili kwa Watumishi wa Umma iliyotolewa na Shaibu Ali, ilisisitiza maadili kama nidhamu, uwajibikaji na heshima kwa Watumishi wa Umma, huku mada ya huduma kwa wateja ikatolewa na Dkt. Amir Mdowe kutoka IPA na kubainisha umuhimu wa lugha nzuri na upokeaji wa Wateja kwa ukarimu, yote yakichangia ufanisi na kuimarisha imani ya Wananchi.
Mafunzo ya kujenga uwezo ya Siku Mbili kwa Wafanyakazi wa Kampuni ya Bima ya ZIC Takaful yameandaliwa na Chuo cha Utawala wa Umma IPA ambapo mada Sita zitawasilishwa katika Mafunzo hayo.

