Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) imefanya zoezi la utayari ikiwa ni sehemu ya majukumu yake ya kawaida ya usalama wa anga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), lenye lengo la kupima uwezo wa kukabiliana na matukio ya dharura yanayoweza kutokea katika Viwanja vya Ndege.
Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Mulhat Yussuf Said, Amewatoa wasiwasi Wananchi ambao waliingiwa na hali ya mshangao, mara baada ya Moshi mzito kuonekana uwanja wa ndege huku Ambulance zikijongea maeneo hayo hali ambayo iliibua taharuki kwa Wananchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari amesema zoezi hilo ni la kawaida na hufanywa kila baada ya muda maalumu kwa lengo la kupima uwezo wa taasisi husika na wadau mbalimbali katika kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea, hususan ajali za ndege.Mulhat ameongeza kuwa zoezi hilo linahusisha vyombo vya ulinzi na usalama, huduma za afya, zimamoto pamoja na taasisi nyingine muhimu, ili kuhakikisha kunakuwa na uratibu wa haraka na madhubuti pale maafa yanapotokea. Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kupuuza taarifa zisizo rasmi, akisisitiza kuwa usalama wa abiria na wafanyakazi wa uwanja wa ndege unaendelea kupewa kipaumbele cha hali ya juu.
