Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amepongezwa na Viongozi mbalimbali waliofika Ikulu Zanzibar kwa sherehe zilizofanywa za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Majeshi ya ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania CDF Jenerali Jacob John Mkunda alipokutana na kufanya mazunguzu na Dkt Mwinyi Ikulu.
Dkt Mwinyi amelishukuru na kulipongeza Jeshi kwa kufanikisha sherehe hizo za Miaka 60 ya Mapinduzi ambapo chini ya uongozi wake Vikosi vya ulinzi na usalama vilipendezesha sherehe hizo kwa Gwaride katika uwanja wa New Amaan Complex.
Amelihakikishia Jeshi la ulinzi kwamba Uchumi wa Zanzibar utanawiri na kuwa tofauti siku zijazo kutokana na Miradi mingi ya maendeleo iliyozinduliwa kuelekea maadhimisho ya sherehe hizo.
Mkuu wa Majeshi ya ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania CDF Jenerali Jacob John Mkunda amesifu juhudi za Dkt Mwinyi na mabadiliko yanayoendana na uchumi kutokana na Miradi iliyozinduliwa.
Aidha Dkt. Mwinyi amekutana na Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje Balozi Stephen Mbundi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje Balozi Said Shaibu Mussa waliofika kujitambulisha.
Dkt. Mwinyi amewaahidi ushirikiano kutoka Zanzibar na kwa upande wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Zanzibar imebadilika na kuwa mshirika katika mikutano mbalimbali.