Raisi wa Jamuhuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea kuunga mkono Mahakama katika kutumia Teknolojia na mifumo ya Kidigitali.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano wa Nchi 56 Wanachama wa Jumuiya ya Madola katika Ukumbi wa Golden Tulip U/ndege Dkt. Samia amesema ni muhimu kwa Sekta za kisheria kutumia teknolojia ili kuhakikisha urahisi na ufanisi katika upatikanaji wa haki kwa wote.
Aidha Dkt. Samia amesema Tanzania inatekeleza mbinu mbali mbali za kukabiliana na matatizo yaliyoainishwa na Mawaziri wa Jumuiya ya Madola katika azimio la 2019 juu ya "usawa katika kuifikia haki" ikiwa ni pamoja na umasikini, gharama kubwa za uwendeshaji wa kesi, lugha ngumu ya kisheria na rushwa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola rt Mhe. Patricia Scotland KC amesema ni muhimu kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya Dunia katika Sekta zote ikiwemo ya sheria kwa kutumia Teknolojia na uvumbuzi ili kuwezesha upatikanaji wa haki sawa kwa wote.
Waziri wa Katiba na sheria wa Jamuhuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Pindi Hazara Chana na Waziri wa Katiba na Sheria Utumishi na Utawala bora Mhe. Haroun Ali Suleiman wamesema Mkutano huo utawawezesha Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo kubadilishana uzoefu katika masuala ya kisheria na mbinu za kukabiliana na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo.
Mkutano huo umehudhuria na Wageni 300 wa Nchi 56 za Jumuiya ya Madola ikiwemo Sri lanka, India, Nigeria, Canada, Mauritius, Rwanda na Kenya wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Sita wa Jumuiya hiyo Mhe. Patricia Scotland KC.