DKT.NDUMBARO AKUTANA NA VIONGOZI WA CHAMUSTA

Mh.Damas Ndumbaro

     WAZIRI wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Maafisa Utamaduni na Sanaa Tanzania (CHAMUSTA) na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo suala la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika jamii, uboreshaji wa mazingira ya utendaji kazi ya maafisa utamaduni pamoja na ubidhaishaji wa urithi wa utamaduni kwa ajili ya utalii wa utamaduni, Malikale na michezo.

     Katika kikako hicho kilichofanyika  Mei 2, 2024 Jijini Dar Es Salaam viongozi hao wamejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na hali mbaya ya mmomonyoko wa maadili ambayo imeelezwa kwa kiasi kikubwa inatokana na urithishaji hafifu wa maadili kutoka kwa wazazi au walezi na jamii kwa ujumla ambapo pia wamemshukuru Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuhamasisha Jamii kuchukua hatua za kukabiliana na suala hilo.

     Aidha, viongozi hao wamejadili juu ya uboreshaji wa hali ya rasilimali watu, mazingira ya utendaji kazi wa Maafisa Utamaduni na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya kisekta katika ngazi za Mikoa na Halmashauri.

    Mhe. Ndumbaro amewataka CHAMUSTA kuandaa mpango kabambe wa kutekeleza kampeni ya kuhamasisha urithishaji wa maadili ili kuongeza uelewa kwa jamii, kuimarisha Zao la utalii wa Utamaduni Malikale na Michezo, pamoja na kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao.

    Naye Mwenyekiti wa Maafisa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Tito Lulandala amemshukuru Mhe. Ndumbaro kwa Ushirikiano, na maelekezo aliyoyatoa kwa Maafisa Utamaduni na Sanaa nchini akieleza kuwa yatakuwa chachu ya Mageuzi makubwa katika utendaji wa Maafisa Utamaduni,  Maendeleo ya Kitengo cha Utamaduni Sanaa na Michezo katika Ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na maendeleo ya sekta husika.

stories
standard
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.